SOMO LA IMANI: “NJOO UWEKE MKONO JUU YAKE, NAYE ATAISHI” MT 9:18

SOMO LA IMANI: “NJOO UWEKE MKONO JUU YAKE, NAYE ATAISHI” MT 9:18

SOMO:

Hos 2:14, 15-16, 19-20

Zab: 145:2-3 4-5, 6-7, 8-9

INJILI:

Mt 9:18-26

NUKUU:

“Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema,” Hos 2:19

“Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana,” Hos 2:20

“Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi,” Mt 9:18

“Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile,” Mt 9:22

 

TAFAKARI: 

“Njoo uweke mkono juu yake, naye ataishi.”

Wapendwa wana wa Mungu, wakati nyakati zilipotimia Mungu aliyekuwa mbali sana katika uelekezaji na utendaji alikuwa Emmanueli yaani, Mungu pamoja nasi (Yoh 1:14, Ebr 1:1-2, Gak 4:4-5). Ukaribu wa ‘Mungu nasi’ ambaye ndiye Yesu Kristo, ni hakikisho la uzima ndani yetu. Mungu wetu ni hai muda wote. Uwepo wa Neno aliyefanyika mwili ni uhai katika miili yetu hii inayokufa. Na hivyo, “Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi,” Mt 9:18. Uhai ndani na katika Kristo unaonekana kwa wote wale waliomridhia. Kristo ndiye kimbilio letu na uhai wetu. “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake,” Mt 9:20. Mwanamke huyu anaona uhai ndani na katika Kristo. Analishika pindo la vazi la Yesu kwa imani na anapona. Naye Yesu anamwambia, “Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile,” Mt 9:22. Je, unaimani thabiti na Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa Maisha yako? Na katika hali ya kufa unashika wapi na nani?

Wapendwa katika Kristo, Bwana wetu Yesu Kristo akiwa njiani kufanya uponyaji, anakutana na taarifa za kuhuzunisha kwamba uhai ule anaoukimbilia haupo tena. Kwa vile yeye ni Bwana wa Uhai na amekuja kwa sababu hiyo ya uhai tena tuwe nao wa kutosha, anasema, “Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu,” Mt 9:24. Kifo ni usingizi tu. Wote wenye kumridhia Mungu wataamshwa kutoka uzingizi wao siku ya mwisho. Je, bado umelala? Amka na mfuate Kristo.

Maisha mapya na yenye matumaini ya kweli twayapata pale tunapokuwa na uhusiano mzuri na Muumba wetu. Fundisho hili ndilo alitoalo Nabii Hosea kwa wana wa Israeli waliokwisha kukata tamaa. Mungu yupo tayari kuanza nasi upya na kusahau historia yetu mbaya, Lk 15:11-32. Agano hili jipya na Mungu lategemea utayari wako. Ukiwa tayari Mungu anasema haya juu yako kama alivyowaambia wana wa Israeli, “Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema,” Hos 2:19. Tendo hili limebebwa katika misingi ya pendo, kweli, haki (ambayo huenda na hukumu), na huruma ya Mungu.

Posa hii yenye kuonyesha upendo wa ndani kati ya mposa-Mungu, na mposwa-mimi na wewe, hudumu katika uaminifu wa kweli. Kumbe yanipasa kuwa kile nilicho kwa nyakati zote na wakati huo nikiutazama ule wokovu kama alama ya mabadiliko yangu ya ndani, yaani, maisha yangu ya kiroho. Mahusiano haya ndiyo sababu na uwezekano wa kumjua Mungu.  Naye Mungu anasema, “Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana,” Hos 2:20. Haya yote yamekamilika ndani na katika Kristo Yesu. Je, maisha yako yamefungamanishwa na upendo wa Kristo ndani yako?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya,” Mt 9:22a

Tusali:-Ee Yesu Kristo nakuamini. Amina

Comments

comments